Mfalme mteule wa Mungu
1 Kwa nini mataifa yanafanya ghasia?
Mbona watu wanafanya njama za bure?
2 Wafalme wa dunia wanajitayarisha;
watawala wanashauriana pamoja,
dhidi ya Mwenyezi-Mungu na mteule wake.
3 Wanasema: “Tujiondoe katika utawala wao;
tutupilie mbali minyororo yao!”
4 Mwenyezi-Mungu atawalaye juu mbinguni,
anawacheka na kuwadhihaki.
5 Kisha, anawakaripia kwa ghadhabu,
na kuwatisha kwa hasira, akisema:
6 “Nimemtawaza mfalme niliyemteua,
anatawala Siyoni, mlima wangu mtakatifu!”
7 Mfalme asema: “Nitatangaza azimio la Mwenyezi-Mungu.
Mungu aliniambia:
‘Wewe ni mwanangu,
mimi leo nimekuwa baba yako.
8 Niombe nami nitakupa mataifa yawe urithi wako,
na dunia nzima kuwa mali yako.
9 Utawaponda kwa fimbo ya chuma;
utawavunja kama chungu cha mfinyanzi!’”
10 Sasa enyi wafalme, tumieni busara;
sikilizeni onyo hili, enyi watawala wa dunia.
11 Mtumikieni Mwenyezi-Mungu kwa uchaji;
12 msujudieni na kutetemeka;
asije akakasirika, mkaangamia ghafla;
kwani hasira yake huwaka haraka.
Heri yao wote wanaokimbilia usalama kwake!