Zaburi 1

Furaha ya kweli

1 Heri mtu asiyefuata shauri la waovu,

asiyeshiriki njia za wenye dhambi,

wala kujumuika na wenye dharau;

2 bali huifurahia sheria ya Mwenyezi-Mungu,

na kuitafakari mchana na usiku.

3 Huyo ni kama mti uliopandwa kando ya vijito,

unaozaa matunda kwa wakati wake,

na majani yake hayanyauki.

Kila afanyalo hufanikiwa.

4 Lakini waovu sivyo walivyo;

wao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.

5 Kwa hiyo watu waovu wataanguka wakati wa hukumu,

wenye dhambi hawatakaa na kusanyiko la waadilifu.

6 Maana Mwenyezi-Mungu huziongoza njia za waadilifu;

lakini njia za waovu zitaishia katika maangamizi.