Jibu la Yobu
1 Hapo Yobu akajibu:
2 “Mambo kama hayo nimeyasikia mengi;
nyinyi ni wafariji duni kabisa!
3 Mwisho wa maneno haya matupu ni lini?
Au ni kitu gani kinachowachochea kujibu?
4 Kama nyinyi mngekuwa mimi, na mimi nyinyi,
ningeweza kusema kama nyinyi
ningeweza kubuni maneno dhidi yenu,
na kutikisa kichwa changu.
5 Ningeweza kuwatia moyo kwa maneno yangu,
na maneno yangu ya faraja yangewatuliza.
6 “Lakini nikisema maumivu yangu hayatulii,
na nikikaa kimya hayaondoki.
7 Kweli Mungu amenichakaza
ameharibu kila kitu karibu nami.
8 Amenifanya ninyauke, na huo ni ushindi dhidi yangu.
Kukonda kwangu kumenikabili
na kushuhudia dhidi yangu.
9 Amenirarua kwa hasira na kunichukia;
amenisagia meno;
na adui yangu ananikodolea macho.
10 Watu wananidhihaki na kunicheka;
makundi kwa makundi hunizunguka,
na kunipiga makofi mashavuni.
11 Mungu amenitia mikononi mwa wajeuri,
na kunitupa mikononi mwa waovu.
12 Nilikuwa nimestarehe, lakini akanivunjavunja,
alinikaba shingo na kunipasua vipandevipande;
alinifanya shabaha ya mishale yake,
13 akanipiga mishale kutoka kila upande.
Amenipasua figo bila huruma,
na nyongo yangu akaimwaga chini.
14 Hunivunja na kunipiga tena na tena;
hunishambulia kama askari.
15 “Nimejishonea mavazi ya gunia,
fahari yangu nimeibwaga mavumbini.
16 Uso wangu ni mwekundu kwa kulia,
kope zangu zimekuwa nyeusi ti;
17 ingawa sijafanya dhuluma kwa mkono wangu,
na sala zangu kwa Mungu ni safi.
18 “Ewe dunia, usiifunike damu yangu iliyomwagika;
kilio changu kienee kila mahali.
19 Nina hakika ninaye shahidi wangu mbinguni,
mwenye kunitetea yuko huko juu.
20 Rafiki zangu wanidharau;
nabubujika machozi kumwomba Mungu.
21 Laiti mtu angenitetea mbele ya Mungu,
kama ifanyikavyo duniani kati za watu wawili.
22 Naam, miaka yangu ni michache,
nami nitakwenda huko ambako sitarudi.