1 Ee Yerusalemu, vua vazi lako la huzuni na mateso,
ukavae milele uzuri wa utukufu wa Mungu.
2 Jivike joho la uadilifu utokao kwa Mungu;
vaa kichwani taji la utukufu wa Mungu wa milele.
3 Maana Mungu atadhihirisha fahari yako kila mahali duniani.
4 Mungu atakupa jina hili milele:
“Amani kwa uadilifu; fahari kwa uchaji wa Mungu.”
5 Inuka, ee Yerusalemu, usimame milimani,
tazama upande wa mashariki,
uwaone watoto wako wamekusanywa kutoka mashariki na magharibi,
kwa amri ya Mungu Mtakatifu.
Wanashangilia kwani Mungu amewakumbuka.
6 Waliondoka kwako kwa miguu,
wakichukuliwa na maadui zako.
Lakini Mungu atawarejesha tena kwako
wakiwa wamebebwa kwa fahari kama juu ya kiti cha enzi cha mfalme.
7 Mungu ametoa amri:
Milima na vilima visawazishwe, na mabonde yafukiwe, nchi yote iwe tambarare,
Waisraeli watembee salama kwa utukufu wa Mungu.
8 Kwa amri ya Mungu,
vichaka na miti itoayo harufu nzuri itawapa kivuli Waisraeli.
9 Mungu atawaongoza Waisraeli kwa furaha;
kwa mwanga wa utukufu wake, kwa uadilifu utokao kwake mwenyewe.