Wimbo wa Tobiti
1 Basi, Tobiti akasema utenzi huu:
“Atukuzwe Mungu aishiye milele,
maana utawala wake wadumu nyakati zote.
2 Yeye huadhibu na kusamehe;
huwaporomosha watu chini katika makao ya wafu,
kisha huwanyanyua humo maangamizini;
hakuna awezaye kuukwepa mkono wake.
3 “Enyi watu wa Israeli, msifuni mbele ya mataifa,
maana kama amewatawanya miongoni mwao,
4 humohumo amewaonesha nyinyi ukuu wake.
Mtukuzeni mbele ya viumbe vyote.
Yeye ni Bwana na Mungu wetu;
yeye ni Baba yetu na Mungu milele na milele.
5 “Ingawa huwaadhibu kwa uovu wenu,
atawahurumieni nyinyi nyote;
atawakusanya kutoka kila taifa
kila mahali mlikotawanywa.
6 “Kama mkimrudia Mungu kwa moyo na roho yote,
mkaishi kwa ukweli mbele yake,
yeye naye atawarudieni
wala hatawaficheni tena uso wake.
7 Kumbukeni jinsi alivyowatendeeni vema,
na kumshukuru kwa sauti.
Mtukuzeni Bwana mwenye haki;
mheshimuni Mfalme wa milele.
8 “Mimi, naimba sifa zake uhamishoni,
nadhihirisha uwezo na ukuu wake
miongoni mwa taifa lenye dhambi.
Enyi wenye dhambi mrudieni Bwana,
fanyeni mambo ya haki mbele yake.
Huenda atawaonesha wema wake
na kuwaoneeni huruma tena.
9 “Kwa upande wangu mimi namtukuza Mungu;
nafsi yangu yashangilia kwake Mfalme wa mbingu.
10 “Kila mmoja na atangaze ukuu wake
na kuimba sifa zake huko Yerusalemu.
“Ewe Yerusalemu, mji mtakatifu,
Mungu amekuadhibu kwa makosa ya watu wako,
lakini atawahurumia watu watendao yaliyo sawa.
11 Mshukuru Bwana maana ni mwadilifu,
mtukuze Mfalme wa milele;
hekalu lake lijengwe upya kwako kwa furaha;
12 awafurahishe watu wako wote walio uhamishoni,
awaangalie kwa upendo wote walio taabuni,
mpaka vizazi vyote vijavyo.
13 “Mwanga mwangavu itaziangaza nchi zote duniani;
mataifa mengi yatakuja kutoka mbali,
wakazi wa nchi zote za mbali duniani
watakuja kulitukuza jina takatifu la Mungu wako.
Watakuja na zawadi kwa mfalme wa mbinguni.
Kwako vizazi na vizazi vitatangaza furaha yao
na jina lako wewe mteule litadumu milele,
katika vizazi vyote vijavyo.
14 Na walaaniwe wote watakaokutisha!
Walaaniwe wote watakaokuharibu na kuangusha kuta zako
wote watakaovunja minara na kuchoma nyumba zako!
Lakini wabarikiwe daima wote watakaokujenga.
15 “Furahi, kwa sababu ya watu wako waadilifu;
maana watakusanywa pamoja kutoka uhamishoni
na kumtukuza Bwana wa nyakati zote.
“Heri yao wote wakupendao
na kufurahia ustawi wako.
16 Heri yao wote wanaohuzunika juu ya adhabu yako
maana watafurahi pamoja nawe upesi,
watashuhudia furaha yako milele.
“Nafsi yangu yamtukuza Mungu, Mfalme mkuu;
17 Maana Yerusalemu utajengwa upya,
na makao yake yatakuwa humo milele.
“Nitakuwa na furaha kiasi gani
wanangu watakapoona utukufu wako
na kumshukuru Mfalme wa mbinguni!
“Milango yako Yerusalemu itatengenezwa
kwa mawe ya johari na zumaridi,
na kuta zako zote kwa mawe ya thamani;
Minara yako itajengwa kwa dhahabu,
na maboma yake kwa dhahabu safi.
Barabara zako zitasakafiwa
kwa mawe ya hakiki na vito vya Ofiri.
18 Malango yako yatajaa nyimbo za shangwe;
na katika nyumba zako zote kutaimbwa:
‘Asifiwe Mungu! Atukuzwe Mungu wa Israeli!’
Kwako Yerusalemu, watalisifu jina lake takatifu
milele na milele.”