Malaki 4

Siku ya Mwenyezi-Mungu inakuja

1 Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema: “Tazama, siku yaja, nayo inawaka kama tanuri. Wenye kiburi na waovu wote watatupwa humo na kuteketea kama mabua makavu; watateketea kabisa pasibaki hata alama.

2 Lakini kwa ajili yenu nyinyi mnaonicha, uwezo wangu wa kuokoa utawachomozea kama jua lililo na nguvu za kuponya kwenye mionzi yake. Mtatoka mkirukaruka kama ndama watokapo zizini mwao.

3 Siku hiyo mtawakanyagakanyaga waovu, nao watakuwa kama majivu chini ya nyayo zenu. Nasema mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi.

4 “Kumbukeni sheria, kanuni na maagizo yangu niliyomwamuru Mose mtumishi wangu kule mlimani Horebu, ili awaamuru watu wote wa Israeli.

5 “Tazama, kabla ya kufika siku ile kuu na ya kutisha, nitamtuma nabii Elia.

6 Nabii Elia atawapatanisha wazazi na watoto wao; la sivyo, nitakuja na kuiangamiza nchi yenu.”