Yona 2

Sala ya Yona

1 Basi, Yona, akiwa tumboni mwa samaki huyo, akawa akimwomba Mwenyezi-Mungu, Mungu wake,

2 akisema:

“Kwa sababu ya taabu yangu,

nilikuomba, ee Mwenyezi-Mungu,

nawe ukanisikiliza;

toka chini kuzimu, nilikulilia,

nawe ukasikiliza kilio changu.

3 Ulinitupa katika kilindi, katikati ya bahari,

gharika ikanizunguka,

mawimbi na gharika vikapita juu yangu.

4 Nilidhani kwamba nimetengwa nisiwe mbele yako;

nisiweze kuliona tena hekalu lako takatifu.

5 Maji yalinizunguka na kunisonga;

kilindi kilinifikia kila upande,

majani ya baharini yakanifunika kichwa.

6 Niliteremka hadi kwenye misingi ya milima,

katika nchi ambayo milango yake imefungwa milele.

Lakini wewe, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu,

umenipandisha hai kutoka humo shimoni.

7 Roho yangu ilipoanza kunitoka,

nilikukumbuka, ee Mwenyezi-Mungu,

sala yangu ikakufikia,

katika hekalu lako takatifu.

8 Watu wanaoabudu sanamu za miungu batili,

huutupilia mbali uaminifu wao kwako.

9 Lakini mimi, kwa wimbo wa shukrani,

nitakutolea sadaka,

na kutimiza nadhiri zangu.

Mwenyezi-Mungu, ndiye aokoaye.”

10 Basi, Mwenyezi-Mungu akamwamuru yule samaki, naye akamtapika Yona kwenye nchi kavu.