1 Enyi Waisraeli, sikilizeni neno Mwenyezi-Mungu alilosema dhidi yenu, enyi taifa zima alilolitoa nchini Misri:
2 “Kati ya mataifa yote ulimwenguni,
ni nyinyi tu niliowachagua.
Kwa hiyo nitawaadhibu nyinyi,
kwa sababu ya uovu wenu wote.”
Jukumu la nabii
3 Je, watu wawili huanza safari pamoja,
bila ya kufanya mpango pamoja kwanza?
4 Je, simba hunguruma porini
kama hajapata mawindo?
Je, mwanasimba hunguruma pangoni mwake
kama hajakamata kitu?
5 Je, mtego bila chambo
utamnasa ndege?
Je, mtego hufyatuka
bila kuguswa na kitu?
6 Je, baragumu ya vita hulia mjini
bila kutia watu hofu?
Je, mji hupatwa na janga
asilolileta Mungu?
7 Hakika, Bwana Mwenyezi-Mungu hafanyi kitu
bila kuwafunulia watumishi wake manabii nia yake.
8 Simba akinguruma,
ni nani asiyeogopa?
Bwana Mwenyezi-Mungu akinena,
ni nani atakataa kuutangaza ujumbe wake?
Kuangamizwa kwa Samaria
9 Tangazeni katika ikulu za Ashdodi,
na katika ikulu za nchi ya Misri:
“Kusanyikeni kwenye milima
inayoizunguka nchi ya Samaria,
mkajionee msukosuko mkubwa
na dhuluma zinazofanyika humo.”
10 Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Watu hawa wameyajaza majumba yao
vitu vya wizi na unyang’anyi.
Hawajui kabisa kutenda yaliyo sawa!
11 Kwa hiyo, adui ataizingira nchi yao,
atapaharibu mahali pao pa kujihami,
na kuziteka nyara ikulu zao.”
12 Mwenyezi-Mungu, asema hivi: “Kama vile mchungaji ampokonyavyo simba kinywani miguu miwili tu au kipande cha sikio la kondoo, ndivyo watakavyonusurika watu wachache tu wa Israeli wakaao Samaria, ambao sasa wanalalia vitanda vizuri na matandiko ya hariri.”
13 Bwana Mungu wa majeshi asema hivi:
“Sikilizeni, mkawaonye wazawa wa Yakobo:
14 Siku nitakapowaadhibu Waisraeli
kwa sababu ya makosa yao,
nitayaharibu pia madhabahu ya mji wa Betheli.
Nitazikata pembeza kila madhabahu
na kuziangusha chini.
15 Nitaziharibu nyumba zote mjini na vijijini;
nitazibomoa nyumba zilizopambwa kwa pembe,
majumba makubwamakubwa hayatasalia hata moja.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”