Kumrudia Mungu na hali mpya
1 Enyi Waisraeli,
mrudieni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.
Mmejikwaa kwa sababu ya uovu wenu.
2 Ombeni toba kwake,
mrudieni na kumwambia:
“Utusamehe uovu wote,
upokee zawadi zetu,
nasi tutakusifu kwa moyo.
3 Ashuru haitatuokoa,
hatutategemea tena farasi wa vita.
Hatutaviita tena: ‘Mungu wetu’
hivyo vinyago tulivyochonga wenyewe.
Kwako ee Mungu yatima hupata huruma.”
4 Mwenyezi-Mungu asema,
“Nitaponya utovu wao wa uaminifu;
nitawapenda tena kwa hiari yangu,
maana sitawakasirikia tena.
5 Nitakuwa kama umande kwa Waisraeli
nao watachanua kama yungiyungi,
watakuwa na mizizi kama mwerezi wa Lebanoni.
6 Chipukizi zao zitatanda na kuenea,
uzuri wao utakuwa kama mizeituni,
harufu yao nzuri kama maua ya Lebanoni.
7 Watarudi na kuishi chini ya ulinzi wangu,
watastawi kama bustani nzuri.
Watachanua kama mzabibu,
harufu yao nzuri kama ya divai ya Lebanoni.
8 Enyi watu wa Efraimu,
mna haja gani tena na sanamu?
Mimi ndiye ninayesikiliza sala zenu,
mimi ndiye ninayewatunzeni.
Mimi nitawapa kivuli kama mberoshi,
kutoka kwangu mtapata matunda yenu.
9 Yeyote aliye na hekima ayaelewe mambo haya,
mtu aliye na busara ayatambue.
Maana njia za Mwenyezi-Mungu ni nyofu;
watu wanyofu huzifuata,
lakini wakosefu hujikwaa humo.”