Hosea 11

Upendo wa Mungu wapita hasira yake

1 “Israeli alipokuwa mtoto, nilimpenda,

Kutoka Misri nilimwita mwanangu.

2 Lakini kadiri nilivyozidi kuwaita,

ndivyo walivyozidi kwenda mbali nami;

waliendelea kuyatambikia Mabaali,

na kuvifukizia ubani vinyago vya miungu.

3 Mimi ndiye niliyemfundisha Efraimu kutembea!

Mimi mwenyewe niliwachukua mikononi mwangu;

lakini hawakutambua kuwa mimi ndiye niliyewatunza.

4 Niliwaongoza kwa kamba za huruma

naam, kwa kamba za upendo;

kama baba amwinuaye mtoto mpaka shavuni mwake,

ndivyo nami nilivyokuwa kwao.

Mimi niliinama chini na kuwalisha.

5 Basi, watarudi nchini Misri;

watatawaliwa na mfalme wa Ashuru,

kwa sababu wamekataa kunirudia.

6 “Upanga utavuma katika miji yao,

utavunjavunja miimo ya malango yake

na kuwaangamiza katika ngome zao.

7 Watu wangu wamepania kuniacha mimi,

wakiitwa waje juu,

hakuna hata mmoja anayeweza.

8 Ewe Efraimu, nawezaje kukuacha?

Nawezaje kukutupa ewe Israeli?

Nitawezaje kukufanya kama mji wa Adma?

Nitawezaje kukutenda kama Seboimu!

Nazuiwa na moyo wangu;

huruma yangu imezidi kuwa motomoto.

9 Nitaizuia hasira yangu kali;

sitamwangamiza tena Efraimu,

maana mimi ni Mungu, wala si binadamu.

“Mimi ndimi Mtakatifu miongoni mwenu,

nami sitakuja kuwaangamiza.

10 “Watanifuata mimi Mwenyezi-Mungu ningurumaye kama simba;

nitakaponguruma watanijia toka magharibi wakitetemeka.

11 Watakuja kutoka Misri wakitetemeka kama ndege,

wataruka kutoka Ashuru kama hua

nami nitawarudisha makwao;

mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.

12 Watu wa Efraimu wananirundikia uongo,

na Waisraeli udanganyifu.

Watu wa Yuda, wananiasi mimi Mungu Mtakatifu.