Toba isiyo ya kweli
1 “ ‘Twendeni, tukamrudie Mwenyezi-Mungu!
Yeye mwenyewe ameturarua,
lakini yeye mwenyewe atatuponya.
Yeye mwenyewe ametujeruhi,
lakini yeye mwenyewe atatibu majeraha yetu.
2 Baada ya siku mbili, atatupa uhai tena,
naam, siku ya tatu atatufufua
ili tuweze kuishi pamoja naye.
3 Basi tumtambue,
tujitahidi kumjua Mwenyezi-Mungu.
Kuja kwake ni hakika kama alfajiri,
yeye atatujia kama manyunyu,
kama mvua za masika ziinyweshayo ardhi.’”
4 Lakini Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Nitakutendea nini ee Efraimu?
Nikufanyie nini ee Yuda?
Upendo wenu kwangu ni kama ukungu wa asubuhi,
kama umande unaotoweka upesi.
5 Ndiyo maana nimewavamia kwa njia ya manabii,
nimewaangamiza kwa maneno yangu,
hukumu yangu huchomoza kama pambazuko.
6 Maana ninachotaka kwenu ni upendo na si tambiko,
Kumjua Mungu na si kutoa sadaka za kuteketezwa.
Uhalifu umeenea kote nchini
7 “Lakini mlilivunja agano langu
kama mlivyofanya mjini Adamu;
huko walinikosea uaminifu.
8 Gileadi ni mji wa waovu,
umetapakaa damu.
9 Kama wanyang’anyi wamwoteavyo mtu njiani,
ndivyo na makuhani walivyojikusanya na kuvizia.
Wanaua watu njiani kuelekea Shekemu,
naam, wanatenda uovu kupindukia.
10 Nimeona jambo la kuchukiza sana
miongoni mwa Waisraeli:
Watu wa Efraimu wanakimbilia miungu mingine
naam, Waisraeli wamejitia unajisi.
11 Nawe Yuda hali kadhalika,
nimekupangia wakati utakapovuna adhabu.